SIMBA KUMFUATA NIYONZIMA
SASA ni rasmi kuwa kiungo wa zamani wa Yanga, Haruna Niyonzima amehamia Simba na atatambulishwa Agosti 8 siku ya sherehe za klabu hiyo, Simba Day.
Uongozi wa Simba umesema jana watampitia Niyonzima kwao Rwanda timu yao itakaporejea Jumamosi kutoka Afrika Kusini ilikopiga kambi kujiandaa na Ligi Kuu ya soka Tanzania bara msimu ujao.
Niyonzima aliyemaliza mkataba na timu yake ya zamani ya Yanga amesaini mkataba wa miaka miwili Simba na kilichobaki ilikuwa kutambulishwa rasmi. Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara alisema jana Dar es Salaam Niyonzima sasa ni mchezaji wao halali wa Simba na wameshamalizana.
“Niyonzima ni mchezaji halali wa Simba. tumeshamalizana naye, anaweza akaenda Afrika Kusini kuungana na kikosi au akawahi kuja au tukampitia Rwanda kwani kikosi kitakuja na RwandAir,”alisema. Alisema mchezaji huyo anatarajiwa kucheza mechi ya kwanza ya kirafiki Simba Day dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Manara alisema mchezaji huyo alichelewa kujiunga na wenzake Afrika Kusini kwa kuwa alikuwa na mambo binafsi anayamalizia Rwanda na kwamba alikuwa akifanya mazoezi na timu ya APR. Manara pia alizungumzia tetesi za beki wao wa kati, Juuko Murshid kwenda Orlando Pirates ya Afrika Kusini akisema bado ni mchezaji wao na ana mkataba hivyo anayemhitaji akazungumze nao.
Alisema wanaendelea na mazungumzo naye kuona namna ya kuboresha mkataba wake. Wakati huo huo, suala la mfadhili wa Simba, Mohamed Dewji kukabidhiwa timu linatarajiwa kupelekwa kwa wanachama kwenye mkutano mkuu Agosti 13, mwaka huu kabla ya mkutano wa kubadilisha Katiba yao Agosti 20, mwaka huu.
Wakati Simba ikiwa kwenye mchakato wa kuzungumza na wanachama, wadhamini wa klabu hiyo walijitokeza kupinga timu kuendeshwa na mtu mmoja wakidai hiyo ni timu ya wanachama wote na si mtu mmoja.
Akizungumzia madai ya Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Klabu, Manara alisema wanachama wana haki ya kutoa maoni lakini wanapaswa kutambua haki hiyo ina kiwango chake na utaratibu wake “Simba ina ‘platform’ ambayo wanachama wana haki ya kuzungumza kutoa maoni yao, kero na ushauri nayo ni mkutano mkuu ambao utasimamiwa na Kamati ya Utendaji kwa sababu viongozi wetu wakuu hawapo lakini wapo wanaokaimu,” alisema.
Manara alisema anawaheshimu wazee hao na kuwaomba kuwa watulivu hasa kipindi hiki cha usajili ambacho wako kwenye maandalizi ya kuanza msimu mpya na Simba Day na kuwataka watumie busara na kuwaacha viongozi wafanye ya muhimu.
Alisema wanahitaji kufanya vizuri msimu ujao kwa kutwaa ubingwa akihoji kuwa watachukuaje kama wanalumbana. Alisema ili kuelekea mabadiliko ya kuingia katika mfumo wa Kampuni na hisa wiki hii wataanza mchakato wa kutoa elimu kwa wanachama wake katika wilaya mbalimbali ili kujua faida zake kabla ya kuitisha mkutano wa Katiba Agosti 20, mwaka huu.
Manara alisema kesho atatoa ratiba kamili ya safari hiyo ya mabadiliko ya kampuni. Alisema Simba imezindua rasmi wiki ya Simba kuelekea kilele cha maadhimisho ya sherehe yao, Simba Day Agosti 8.
Hii ni mara ya pili Simba kuadhimisha siku hiyo iliyoanzishwa mwaka jana. Mwaka huu wataitumia kusaidia jamii na kutembelea makundi maalumu na kuwapa misaada. Akizungumzia siku hiyo jana, Mkurugenzi wa EAG Group, mshauri wa masoko na biashara Simba, Imani Kajura alisema katika kuadhimisha siku hiyo watafanya matukio ya kijamii wakianza na leo watakapozindua huduma mtaa kwa mtaa.
No comments