WENYE VYETI VYA DARASA LA SABA WAANZA KUONDOLEWA SERIKALINI
WENYE VYETI VYA DARASA LA SABA WAANZA KUONDOLEWA SERIKALINI
WATUMISHI wa umma waliodanganya kuwa na vyeti vya kidato cha nne na ambao hawajaviwasilisha kwa waajiri wao, ambao miongoni mwao wana vyeti vya darasa la saba, wameanza kuondolewa katika utumishi wa umma.
Tayari baadhi ya taasisi za umma zimeanza kuwaondoa watumishi hao, kutekeleza agizo la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, inayotaka watumishi hao wanaidai kuwa na elimu ya kidato cha nne, lakini hawajawasilisha vyeti au walisoma darasa la saba, kuondolewa katika malipo kuanzia mwezi huu.
Akizungumza na gazeti hili jana jioni kwa simu, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro alikiri kutolewa agizo la kuwaondoa katika mishahara watumishi hao ambao hawajawasilisha vyeti vyao vya kidato cha nne.
“Hao siyo wa darasa la saba, ni waliojifanya wamefika kidato cha nne lakini hadi sasa hawajawasilisha vyeti vyao. Sheria pia ilitaka kuanzia mwaka 2004 watumishi wenye kidato cha nne ndio waajiriwe kwenye utumishi, sasa kama wapo walioingia kwa upendeleo au kwa makusudi, ndio tumeagiza mwisho wa mwezi huu wasitishiwe mishahara yao,” alifafanua Dk Ndumbaro.
Dk Ndumbaro alieleza kuwa watumishi hao si wengi, kama wale waliogundulika kughushi vyeti hivyo vya elimu ambao walikuwa 9,932, na kwamba idadi yao itajulikana mwishoni mwa mwezi huu wakati waajiri watakapowasilisha taarifa zao.
Imebainika kuwa wafanyakazi 38 kati ya 150 wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu (CDA) waliohamishiwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma wameondolewa kazini kwa kuwa na vyeti vya darasa la saba.
Aidha, taarifa kutoka ndani ya Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani zinaeleza kuwa watumishi zaidi ya 100 wameondolewa kutokana na kuwa na elimu ya darasa la saba. “Shirika likiwa na wafanyakazi ambao walikuwa kwenye miradi mbalimbali, mfano miradi ya ufugaji na ajira zao za awali zilikuwa miezi mitatu mitatu.
“Mwaka 2006 watumishi wengi waliondolewa kwenye mfumo wa ajira ya muda mfupi na kupewa ajira ya kudumu, na kufuatia miradi mingi kufa, wafanyakazi wengi walihamishiwa maeneo mengine hususani hospitalini ambako walitawanywa kwenye vitengo na kufanya kazi pasipokuwa na ujuzi na elimu ya masuala ya afya.
“Sasa kutokana na agizo la kuwaondoa wale wenye elimu ya darasa la saba ambao hawajajiendeleza na waliajiriwa kuanzia mwaka 2004, watumishi zaidi ya 100 wamekumbwa na baadhi walikuwa wanakaribia kustaafu,” kinasema chanzo cha habari. Uongozi wa shirika hilo umeahidi kulizungumzia suala hilo leo.
Wafanyakazi hao wameondolewa kazini kutokana na waraka wa serikali ulilotolewa mwaka 2004, kwamba watumishi wa sekta mbalimbali wajiendeleze kimasomo na wawasilishe vyeti vyao vya kujiendeleza, lakini wao hawakujiendeleza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi alisema wafanyakazi 38 wameondolewa na wao kama halmashauri wanangoja utaratibu mwingine kutoka serikali namna ya kujaza nafasi hizo.
Alisema kuna pengo la wafanyakazi wa kada mbalimbali katika halmashauri yake, hivyo kuondolewa kwa hao, kumeongeza pengo hilo, lakini utaratibu wa namna ya kujaza, wanaiachia serikali.
Alisema uhaba wa wafanyakazi wa sekta mbalimbali ikiwamo ya ardhi aliueleza kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alipozungumza na wafanyakazi iliyokuwa CDA.
Alisema ni kweli kwamba halmashauri hiyo ina uhaba wa wafanyakazi kutokana na kuondolewa hewa na wenyeviti feki na sasa hao wa darasa la saba, lakini wanasubiri serikali kutoa maelekezo ya namna ya kujaza nafasi hizo.
Kutokana na watumishi hao kutotekeleza waraka wa serikali watumishi wa kada ya afya, elimu na nyingine ambao hawakujiendeleza Manispaa ya Dodoma, wamewaondolewa kwenye orodha ya mishahara ya Julai.
No comments