MAHAKAMA YARUHU KUAPISHWA WABUNGE WAPYA CUF
Mahakama yabariki kuapishwa kwa wabunge wapya CUF
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi ya wabunge wanane wa Chama cha Wananchi (CUF) waliovuliwa wadhifa huo walioomba mahakama itoe zuio kwa Bunge kuwaapisha wabunge wapya hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa, kwa kuwa walitumia kifungu cha sheria kisicho sahihi.
Kutokana na uamuzi huo, muda wowote Bunge litakapowahitaji wabunge hao wateule wa viti maalumu walioteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuapishwa, linaweza kufanya hivyo. Akisoma uamuzi huo jana, Jaji Lugano Mwandambo alisema upande wa Serikali uliwasilisha pingamizi tatu dhidi ya maombi hayo ikiwemo la upungufu wa kisheria ambayo yaliwasilishwa na waombaji.
Alisema waombaji walitumia sheria ya Uingereza bila kuambatanisha kifungu cha sheria za hapa nchini ambacho kinaruhusu maombi hayo kusikilizwa mahakamani hapo. Alisema wanakubaliana na pingamizi zilizotolewa na upande wa Serikali hususani lililoonesha kwamba waombaji wametumia kifungu kisicho sahihi, hivyo wanatupilia mbali maombi hayo.
Wakili wa Bodi ya Wadhamini wa CUF, Mashaka Ngole alidai kuwa kesi ya msingi itasikilizwa Septemba 30 mwaka huu na kwamba bado hawajapeleka utetezi wao, pia wataangalia ni gharama gani walizotumia kwa ajili ya kesi hiyo ili waweze kulipwa kwa usumbufu waliopatiwa. Kabla ya kesi hiyo kutolewa uamuzi, saa 4 asubuhi wanaodaiwa kuwa wanachama wa CUF upande wa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na wale wanaomuunga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif Shariff Hamad walianza kurushiana makonde mahakamani hapo huku sababu za kupigana kwao hazikufahamika.
Kutokana na hali hiyo, askari polisi zaidi ya sita waliokuwa mahakamani hapo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi walifika katika ukumbi wa mahakama hiyo na kuanza kuzungumza na wanachama hao kwa lengo la kupunguza ghasia na baadaye hali ilirudi kuwa shwari. Awali, wakati wa kusikilizwa maombi hayo, miongoni mwa pingamizi zilizowasilishwa na Malata ni kuwa kuwa maombi hayo hayatekelezeki kwa kuwa yanalenga kuzuia majukumu ya Bunge ambayo yameainishwa kwa mujibu wa Ibara ya 68 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Malata ambaye alikuwa akiongoza jopo la mawakili wa serikali, alidai waombaji hao wanatumia mamlaka za aina mbili kupata haki zao mojawapo ni kupitia utaratibu wa kichama ambapo walikata rufaa ndani ya Mkutano Mkuu kupinga maamuzi ya baraza na pia wanatumia mahakama kutafuta haki hizo hizo ambazo wangeweza kuzipata kupitia chama chao.
Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alipinga hoja zilizotolewa na upande wa Serikali akidai kuwa hazina msingi kwa kuwa kifungu cha sheria ambacho wateja wao waliegemea kuleta maombi hayo, kinaipa mamlaka mahakama kutoa maamuzi. Waombaji katika kesi hiyo ambao walikuwa wabunge kabla ya kuvuliwa uanachama na kupoteza nafasi hizo ni Miza Bakari, Savelina Mwijage, Salma Mohammed, Raisa Abdallah na Riziki Mngwali, Hadija Salum Al- Qassmay, Halima Ali Mohamed na Saumu Heri Sakala wakati madiwani ni Elizabeth Magwaja na Layla Hussein.
Katika maombi hayo wadaiwa ni Bodi ya Wadhamini wa CUF, Tume ya Uchaguzi (NEC), katibu wa Bunge na wabunge wapya walioteuliwa na NEC. Julai 27 mwaka huu, NEC kwa mujibu wa Ibara ya 78(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na kifungu cha 86(8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343, iliwateua Rukia Kassim, Shamsia Mtamba, Kiza Mayeye, Zainab Mndolwa, Hindu Mwenda, Sonia Magogo, Alfredina Kahigi na Nuru Bafadhili kuwa wabunge wa Viti Maalumu katika Bunge la Muungano, wakichukua nafasi ya waliofukuzwa na chama chao.
Jana jioni, saa chache baada ya uamuzi wa Mahakama, upande wa wabunge waliotimuliwa CUF na kuvuliwa ubunge, kupitia Wakili Kibatala waliwasilisha maombi mapya Mahakama Kuu kulizuia Bunge lisiwaapishe wabunge wapya. Katika maombi hayo, wameongezwa walalamikiwa ambao ni Wakurugenzi wa Manispaa za Temeke na Ubungo, kutokana na madiwani wawili waliokuwa miongoni mwao kutimuliwa.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad amekwama kutimiza azma ya kuwaondoa bungeni wabunge wawili wa chama hicho, Magdalena Sakaya wa Kaliua na Maftaha Nachuma wa Mtwara Mjini, baada ya taarifa ya Spika jana kueleza kuwa, anasita kuifanyia kazi barua ya Maalim Seif ya kuwatimua wabunge hao kutokana na taarifa za awali alizopokea kuonesha kuwa, kuna mabadiliko ndani ya uongozi wa chama hicho yanayomtambua Sakaya kuwa ndiye anayetekeleza majukumu ya Katibu Mkuu wa chama hicho kwa sasa, badala ya Maalim Seif.
“Ofisi ya Spika inayo barua ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha CUF, Profesa Ibrahimu Haruna Lipumba yenye Kumbukumbu Namba CUF/AK/DSM/ MKT/05/2017 ya Machi 22, 2017 ikiliarifu Bunge kuwa Maalimu Seif Shariff Hamad ameshindwa kutekeleza majukumu yake kama Katibu Mkluu, hivyo kwa mujibu wa Katiba ya CUF, majukumu ya Katibu Mkuu yanatekeleza kuanzia tarehe hiyo na Magdalena Sakaya,” imesema sehemu ya barua hiyo. Aidha, imesema barua hiyo ilikuwa na kiambatanisho cha ridhaa ya mabadiliko hayo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na kwamba Ofisi ya Spika haijawahi kupokea barua yoyote ikieleza vinginevyo
No comments