JPM ASABISHA KUSHUKA KWA ADA VYUO VIKUU
Agizo la rais JPM lashusha ada vyuo vikuu
Hata hivyo, imebainika kuwa neema hiyo ya punguzo la ada ni mwiba kwa wamiliki wa vyuo ambao sasa, baadhi yao wamelazimika kufanya kazi ya ziada ili kukabiliana na athari za kupungua kwa mapato ya ada hadi asilimia 25.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa mbali na kushushwa kwa ada, baadhi ya vyuo vimelazimika pia kuondoa gharama za uchukuaji fomu, hivyo kuzitoa bure kwa waombaji ili kuwavutia zaidi.
Katika baadhi ya vyuo, sababu kubwa ya kupunguza ada imetajwa kuwa kuwaongezea fursa Watanzania wenye sifa kujiunga zaidi na vyuo kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu.
Aprili 15 mwaka huu, Rais John Magufuli, alipokuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa mabweni mapya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema utaratibu wa sasa wa kuwapangia vyuo wanafunzi unawachanganya na hivyo unapaswa kuachwa.
“Ninaamini kama wanafunzi wangepewa nafasi ya kuchagua vyuo wanavyovipenda wenyewe, vyuo vya serikali kama vile UDSM, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Chuo Kikuu cha Mzumbe vingekuwa na wanafunzi wengi sana,” alisema.
Rais Magufuli alisema TCU imekuwa ikiwachagulia wanafunzi vyuo visivyo na sifa na makazi ya wanafunzi hivyo kusababisha wanafunzi hao kusoma katika mazingira magumu na wanapomaliza masomo yao kukosa ajira kutokana na vyuo hivyo kutokuwa na sifa.
HALI ILIVYO
Nipashe ilitembelea tovuti za vyuo mbalimbali na kuona baadhi yake vikiwa na punguzo la ada la kati ya Sh. 500,000 hadi 800,000.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCo), Prof. Uswege Mlinga, alisema chuo chake kimepunguza ada kutoka Sh. milioni 2.4 hadi milioni 1.85.
“Tumeamua kupunguza kwa sababu tumeona elimu yetu ni bora lakini tunaweza kupoteza wanafunzi … tukaona afadhali tupunguze kidogo ili tusipoteze wanafunzi wanaopenda kusoma,” alisema.
Aidha, alisema miaka ya nyuma walikuwa wanashindwa kupata wanafunzi wa uhakika kwa sababu wanatakiwa kuomba moja kwa moja.
“Kipindi cha nyuma cha kuomba kupitia TCU, waliangalia chuo, wakati ule ilikuwa wamesikia TUDARCo na wanapewa kwa jinsi alivyochagua. Sasa hivi wanatembelea tovuti mbalimbali na kulinganisha chenye unafuu,” alibainisha.
Prof. Mlinga alisema sababu nyingine ya kupunguza ada ni wanafunzi wengi kuahirisha mitihani kutokana na kushindwa kulipa ada husika.
“Tumekutana na tatizo hili. Wanafunzi wengi wanashindwa kufanya mitihani kwa kukosa ada. Wanaahirisha mitihani, tunafikiri hili litasaidia. Tunataka kuwasaidia wanafunzi,” alisema.
Mkuu huyo alisema pamoja na kwamba itasumbua kwenye bajeti yao, lakini watapunguza matumizi ambayo kwa kiasi kikubwa hayataathiri ufundishaji.
Kuhusu wanafunzi wanaoendelea, Prof. alisema wanasubiri ruhusa ya bodi ambayo imepelekewa mapendekezo ya kupunguza na hivi karibuni itajulikani.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Stephano Moshi (SMMUCO), Mchungaji Dk. Emmanuel Kileo, alisema chuo hicho, baada ya kuona wanafunzi wengi wanashindwa kufanya mitihani kwa sababu ya kukosa ada, kimepunguza ada tangu Februari mwaka huu.
“Ada imepungua kutoka Sh. mil 1.7 hadi milioni 1.2. Tumegundua familia nyingi haziwezi kulipa. Wanafunzi wengi wameshindwa kulipa, wanaishia kwenye kiasi hicho. Tumewasaidia kwa kuondoa kiasi cha Sh, 500,000,” alisema.
Alisema mwaka jana chuo hicho kilitangaza udhamini wa Sh. 500,000 kwa kila mwanafunzi, wakapokea maombi mengi na kushindwa kuyamudu na kuona umuhimu wa kuondoa kiasi hicho.
“Kuna wanafunzi wamemaliza chuo lakini hadi sasa tumeshikilia vyeti vyao kwa kuwa wameshindwa kulipa ada, wanashindwa kutafuta kazi kwa sababu hawana vyeti. Hili siyo lengo la elimu,” alisema.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ualimu Mwenge, Dk. Eugen Lyamtani, alisema chuo hicho kimekuwa na ada nafuu siku zote baada ya kubaini wanafunzi wengi wanashindwa kumudu.
“Ada yetu haijawahi kupanda kwa shahada ya masomo ya Sayansi ni Sh. milioni 2.8 na kwa sanaa ni Sh. milioni 1, pia fomu za kuomba kujiunga na chuo zinatolewa bure,” alisema.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Prof. Faustine Bee, alisema kupunguza ada kwa vyuo vikuu ni mtazamo wa kuvutia wanafunzi na kwamba kwa chuo hicho, ada ni Sh. milioni 1.1 kwa shahada ya kawaida.
“Vyuo vya umma vinaendeshwa kulingana na makusanyo ya ada. Sisi tulichoondoa ni ada ya fomu za kujiunga na chuo ambayo ni Sh. 10,000 na mwanafunzi anailipa baada ya maombi yake kupokelewa na kuonekana ana sifa za kujiunga,” alifafanua.
No comments