JIFUNZE JINSI YA KUANDIKA (CURRICULUM VITAE "CV") KWENYE MAOMBI YA KAZI
JINSI YA KUANDIKA CV IKIWA HAUNA UZOEFU WA KAZI
(WORK EXPERIENCE)
Umemaliza chuo, ni wakati wako wa kuingia kwenye ulimwengu halisi na kupata kazi. Kufanikisha hili, unahitaji uwe na CV itakayo kuuza kwa waajiri, itakayoonyesha maadili ya kazi uliyonayo na jinsi gani utakuwa mfanyakazi utakayejituma.
Lakini unaposoma matangazo mengi ya kazi katika sekta yako unajikuta kuwa unakidhi vigezo vingi vilivyowekwa isipokuwa kile cha ‘uwe na uzoefu wa kazi usiopungua muda flani’, na kujikuta njia panda kutokana na ukweli kwamba, unahitaji kazi ili kupata uzoefu, lakini ukihitajika uwe na uzoefu ili kupewa kazi.
Kwa bahati nzuri, uzoefu ambao waajiri wengi wanauhitaji haupatikani tu kupitia ulimwengu wa ajira rasmi, na kwahiyo, mbinu ya kuandika CV bila ya uzoefu wa kazi rasmi ipo katika kutumia njia za kibunifu kuonyesha una ujuzi unaoweza kuhamishwa kwaajili ya kazi unayoomba na kumshawishi mwajiri kutazama zaidi kile unachoweza kufanya kuliko kile ambacho umeshawahi kufanya.
Hivyo basi, unaweza vipi kuwasilisha CV yako bila ya uzoefu wa kazi? Fanya yafuatayo;
1. ONYESHA UWEZO WAKO..
Kama nilivyotangulia kusema, waajiri hawaangalii tu kile ulichokifanya lakini pia unachoweza kufanya. Hivyo ni lazima uwashawishi kuwa una uwezo wa kuchukua kazi unayoomba.
Ikiwa wewe ni muhitimu mpya wa masomo ya kompyuta au biashara kwa mfano, jiulize kama ulifanya mafunzo kwa vitendo (field au internship) wakati wa masomo yako? Je, umeshawahi kufanya kazi katika kampuni ya rafiki, ndugu au jamaa hata kwa muda mfupi? Unaweza kuyatumia yote hayo katika kuonyesha una uzoefu wa kazi.
2. ANZA CV YAKO KWA TAARIFA BINAFSI..
Hii itakuwa sehemu ya kwanza kabisa mwajiri yoyote kuisoma, hivyo hakikisha haina makosa. Cha muhimu, ifanye fupi na rahisi iwezekanavyo na iwe na angalau maneno 150 pekee.
Anza kwa kujitambulisha mwenyewe, kiwango cha elimu yako pamoja na ujuzi. Unaweza pia kuongeza shahada au masomo uliyoyasoma ukiwa chuo endapo yanaendana na yataongeza mvuto kulingana na aina ya majukumu katika kazi unayoomba.
Hakikisha unaweka pia nafasi unayotafuta. ikiwa unaomba kwenye jukumu moja pekee, basi unaweza kuandika mahususi - "Natafuta nafasi katika upande kwa masoko" n.k. - lakini ikiwa una chaguo pana, andika kwa ujumla - “Natafuta nafasi katika sehemu ambayo naweza kuongeza mchango wangu”.
3. ORODHESHA UJUZI BADALA YA MAJUKUMU..
Tengeneza orodha ya ujuzi wako, na uonyeshe kwa mifano. Ikiwa unataka kusema una ujuzi wa uongozi, basi unaweza kuzungumza kuhusu tukio uliloliandaa au kulisimamia. Lakini pengine wewe ni mzuri katika mawasiliano au mauzo, basi toa mfano wa jinsi gani hili lilikusaidia katika masomo yako na jinsi gani unadhani litakusaidia katika kazi yako unayoomba.
4. ELEZA MAFANIKIO YAKO..
Ongea kuhusu mafanikio yako katika mazingira tofauti kama vile utafiti, masomo au hata burudani endapo inaendana na aina ya kazi unayoomba. Kwa kuzungumza juu ya mafanikio yako unasisitiza ujuzi na uzoefu wako.
Pia onyesha kuwa una ufahamu na uelewa wa kutosha kuhusu kinachotokea katika sekta ya kazi unayoomba, na orodhesha kama umeshawahi kusoma majarida kuhusu sekta hiyo au kushiriki katika midahalo au majadiliano ya ana kwa ana au kwa njia ya mtandao.
5. ZIFANYE SHUGHULI ZAKO ZA ZIADA KAMA KAZI..
Kwa sababu tu ulifanya shughuli yoyote bila kulipwa haimaanishi kuwa haukupata ujuzi muhimu. Yaweke majukumu yako ya kazi za kujitolea sawa na majukumu ya ajira – onyesha muda ulioutumia, majukumu uliyofanya na ujuzi ulioupata.
Panga shughuli zako za ziada kutokana na vipaombele vya kazi, mfano, kama unaomba kazi ya uandishi katika gazeti, mwajiri atahitaji kufahamu zaidi kuhusu makala ulizokuwa unaandika kwenye majarida ya chuo kuliko uhodari wako katika michezo. Kwahiyo kuwa muangalifu juu ya shughuli gani ya ziada unaiweka kwenye CV yako kutokana na kazi unayoiomba.
6. CHEZA VEMA NA ELIMU YAKO..
Ikiwa uliandika utafiti (research) kama sehemu ya masomo yako, basi unaweza kuzungumza juu ya uwezo wako wa kufanya utafiti. Ikiwa ulifanya mawasilisho (presentation), pia unaweza kudai kuwa na uzoefu wa kuzungumza mbele za watu. Jumuisha pia, uzoefu ulioupata katika mradi wa kikundi (group project), kama vile uwezo wa kupanga, au ujuzi wowote unaohusiana na jukumu lako katika mradi.
Mara nyingi wahitimu wengi wanashindwa kuelezea sifa zao na ujuzi kwa namna ambayo ina maana kwa waajiri kwa kutoeleza sababu ya kuajiriwa kwao, na jinsi gani wanaweza kusaidia kampuni au taasisi husika. Kwa mfano, wanaweza kutaja kwenye CV kuhusu tafiti walizoziandika ambazo maudhui yake pengine hayaendani hata na kazi wanazoziomba.
Lakini ikiwa utasema una ujuzi wa kufanya utafiti na kwahiyo utaweza kuandika nyaraka ambazo zitasaidia mawasiliano kwenye idara mbalimbali za kampuni au taasisi, utapokea majibu chanya zaidi kutoka kwa mwajiri. Msingi wake ni kuzingatia kuhusianisha kile ulichokifanya awali, unachokifahamu au kuwa na uzoefu nacho na kazi unayoiomba.
Usifanye kosa la kuacha nafasi tupu kwenye CV yako kwa sababu tu unakosa uzoefu wa kazi. Sehemu ya uzoefu wa kazi katika CV yoyote ile ni njia tu ya kuonyesha jinsi uzoefu uliopita huko nyuma unavyoweza kufaa kwa mwajiri wa baadaye.
MFANO WA CV PAKUA (DOWNLOAD) HAPA CHINI
MAGOPEJR.BLOGSPOT.COM
Naomba kama hutojali uattach video yangu nikionesha namna ya kuandika cv kwa kutumia simu ya mkononi tafadhali
ReplyDeleteLink yake hii hapa chini
https://youtu.be/l3JEl78gMso
Natanguliza shukran